Wajapan wavutiwa na chai ya Tanzania
Wataalamu katika sekta ya chai kutoka nchini Japan waliopo hapa nchini kwa siku saba wakiangazia fursa za uwekezaji katika sekta hiyo wamevutiwa na mafanikio waliyokutana nayo katika sekta ya chai.
Wajapan hao watano wakiongozwa na Bw. Hirofumi Suganuma ambaye ni Mkurugenzi wa Miradi ya Maendeleo, Kampuni ya Kawasaki Kiko ya Japan wametembelea mikoa ya Iringa na Njombe.
Wakiwa mkoani Njombe wametembelea shamba la kibena pamoja na kiwanda cha Lipton kabla ya hapo walitembelea shamba Chama cha Ushirika cha Mkonge kilichopo Mufindi na kuzungumza na wakulima.
Wajapan hao wameongozana na ujumbe wa Bodi ya Chai Tanzania(TBT) pamoja na wataalamu kutoka wizarani katika ziara yao hiyo yote.
Wakiwa katika Kituo cha Utafiti wa Chai Tanzania(TRIT) Wajapan walijionea uwezo mkubwa wa utafiti wa kituo hicho ambapo kimefanya tafiti na kuzalisha majani ya chai ambayo wajapan hao wamevutiwa nayo kwa kuwa yanasaidia katika uzalishaji wa green tea.
Kaimu Mkurugenzi wa TBT, Bi.Beatrice Banzi anasema ziara hiyo imekuwa ya mafanikio kwa kuwa Wajapan hao wamejionea mafanikio katika sekta hiyo na kwa kuwa ni kampuni kubwa katika sekta ya chai, ni wazi kuwa watakuwa na mchango chanya katika sekta hiyo