BODI YA CHAI YAIPA SEKTA YA CHAI MSUKUMO MPYA 2026.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Chai Tanzania (TBT) Bw. AbdulMajid Nsekela, ameongoza kikao cha robo ya pili cha Bodi kwa mwaka 2026 kilichowakutanisha wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya Bodi kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi na kuweka mwelekeo wa maendeleo endelevu ya sekta ya chai nchini.
Kikao kimejadili kwa kina mikakati ya kuendeleza uzalishaji masoko na ubora wa chai ya Tanzania ili kuongeza ushindani wake katika soko la ndani na kimataifa sambamba na kuzingatia maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha uchumi kupitia sekta za uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao ya biashara.
Mwenyekiti wa Bodi amesisitiza umuhimu wa kuongeza ubunifu (innovation) katika tasnia ya chai kufuatilia mwenendo wa masoko ya kimataifa na kuimarisha matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija kwa wakulima, viwanda na wafanyabiashara wa chai. Aidha amelekeza Menejimenti kuhakikisha maslahi ya wakulima yanazingatiwa kikamilifu kwa kuboresha mifumo ya uzalishaji na masoko.
Kikao kimeeleza dhamira ya Bodi ya Chai Tanzania ya kuunga mkono kikamilifu jitihada za Rais Samia za kuimarisha diplomasia ya kiuchumi kuongeza ajira na kukuza matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini ikiwemo chai kama sehemu ya kujenga uchumi imara na shindani.
Kwa ujumla, kikao cha kwanza cha Bodi kwa mwaka 2026 kimeweka msingi imara wa utekelezaji wa mikakati itakayochochea ukuaji wa sekta ya chai kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa na kuinua maisha ya wakulima na wadau wote wa mnyororo wa thamani wa zao la chai nchini.