BODI YA CHAI YAKUTANA NA WADAU KUIMARISHA SEKTA YA CHAI
Bodi ya Chai Tanzania imeendelea kutekeleza dhamira yake ya kushirikiana na wadau wa sekta ya chai kwa lengo la kuimarisha uzalishaji, kuongeza ushindani na kuboresha maslahi ya wakulima na wananchi kwa ujumla. Katika muktadha huo, Bodi imefanya kikao na wachakataji wa viwanda vya chai pamoja na wakulima wakubwa wa chai nchini.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bi. Beatrice Banzi, kimewakutanisha wadau wakuu wa sekta hiyo wakiwemo RBTC, BPTL, SHF, UWL, EUTCO, KTCL, WTC, MHCL na TAT, kwa lengo la kubadilishana mawazo, kujadili changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya pamoja itakayochochea ukuaji endelevu wa sekta ya chai nchini.
Katika kikao hicho wadau wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu gharama za uzalishaji ikiwemo changamoto ya upatikanaji wa umeme katika viwanda vya chai. Aidha, kikao kimeweka msisitizo mkubwa juu ya umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala kama mkakati wa kupunguza gharama za uzalishaji, kulinda mazingira na kuhakikisha sekta ya chai inakuwa endelevu.
Bodi ya Chai Tanzania imesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ni rafiki kwa mazingira ni nguzo muhimu katika kuijenga sekta ya chai yenye tija ushindani na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
Vilevile kikao kimesisitiza umuhimu wa kuimarisha mfumo wa bei ya majani mabichi (Green Leaf Pricing) kwa kuzingatia maeneo ya uzalishaji hali ya miundombinu pamoja na gharama halisi za uzalishaji, huku wadau wakikubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na upatikanaji wa mitaji kwa wadau wa sekta ya chai.
Akizungumza katika kikao hicho Bi. Banzi amewahimiza wadau kuendelea kuwekeza katika ubora wa chai kuchangamkia fursa za masoko ya kimataifa zinazotafutwa na Bodi ya Chai Tanzania, pamoja na kuongeza juhudi za kuhamasisha matumizi ya chai ndani ya nchi. Hatua hiyo itaongeza ajira, mapato na ustawi wa wananchi, sambamba na kukuza uchumi wa taifa.
Juhudi hizi ni sehemu ya mkakati wa Bodi ya Chai Tanzania katika kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, shindani na unaojali mazingira, huku maendeleo yakimnufaisha mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla