Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

BODI YA CHAI TANZANIA

TAMASHA LA CHAI AMSTERDAM LAFUNGUA MASOKO MAPYA KWA CHAI YA TANZANIA.

Imewekwa: 03 Feb, 2026
TAMASHA LA CHAI AMSTERDAM LAFUNGUA MASOKO MAPYA KWA CHAI YA TANZANIA.


Tamasha la Chai la Amsterdam limefanyika kwa mara ya kwanza likiwaalika wadau wa sekta ya chai kutoka nchi zote duniani zinazolima zao hilo zikiwemo Tanzania, Sri Lanka, Japani na Indonesia. Lengo la tamasha hilo lilikuwa kuwakutanisha wazalishaji wa chai ili kubadilishana uzoefu kutambua ubora wa chai wanazozalisha na kutangaza mnyororo wa thamani wa zao la chai katika soko la kimataifa.

Kupitia ushiriki wake katika tamasha hilo, Bodi ya Chai Tanzania imefanikiwa kuitangaza chai ya Tanzania kimataifa kuonesha fursa zilizopo katika sekta ya chai na kuvutia wawekezaji kuwekeza nchini, hususan katika uzalishaji, usindikaji na biashara ya chai.

Aidha, banda la Bodi ya Chai Tanzania lilitembelewa na Balozi wa Indonesia na Balozi wa Sri Lanka nchini Tanzania ambapo walipata fursa ya kuonja chai zinazozalishwa nchini na kushuhudia ubora wake hatua iliyoimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya chai.

Kupitia tamasha hilo, Bodi ya Chai Tanzania imejifunza umuhimu wa diversification (utoaji wa bidhaa za chai za aina mbalimbali), matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na mbinu bora za ufungashaji kulingana na mahitaji ya masoko.

Wageni waliotembelea banda la Tanzania waliipa sifa kubwa chai ya Kilolo, wakieleza kuwa ni chai yenye nguvu, ladha nzuri, harufu ya kuvutia na rangi nzuri, hivyo kuonesha ushindani wa chai ya Tanzania katika soko la dunia.

Bodi ya Chai Tanzania inaushukuru Ubalozi wa Tanzania Nchini Uholanzi kwa mwaliko na maandalizi mazuri yaliyowezesha ushiriki wenye tija, uliosaidia kuitangaza chai ya Tanzania kimataifa na kufungua fursa za ushirikiano na uwekezaji katika sekta ya chai.