BODI YA CHAI YAFANYA KIKAO KAZI KATIKA VIWANDA VYA CHAI MUHEZA
Bodi ya Chai Tanzania imefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kusikiliza na kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya chai kwa lengo la kulinda maslahi ya wakulima, wafanyakazi na wadau wa tasnia ya chai.
Katika ziara hiyo, Bodi ya Chai ilikutana na uongozi na Menejimenti ya Kampuni ya East Usambara Tea Company (EUTCO), pamoja na uongozi wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Chai Amani. Kikao hicho kilijadili kwa kina masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya sekta ya chai, yakiwemo ucheleweshaji wa malipo kwa wafanyakazi na wakulima, pamoja na changamoto za kiutendaji zinazokwamisha ukuaji wa sekta hiyo.
Kikao kimebaini kuwa ucheleweshaji wa malipo ni changamoto kubwa inayohitaji hatua za haraka. Kufuatia mjadala huo, Kampuni ya EUTCO imeahidi kulipa madai yote yaliyosalia kwa wafanyakazi na wakulima kabla au ifikapo tarehe 31 Januari 2026, hatua inayotarajiwa kurejesha imani na ustawi wa wahusika wa sekta ya chai katika eneo hilo.
Aidha, changamoto nyingine zilizojadiliwa ni pamoja na kukatika kwa umeme mara kwa mara, mzigo wa kodi na tozo mbalimbali, pamoja na miundombinu duni, ambazo kwa pamoja zimeendelea kuathiri uzalishaji na ufanisi wa sekta ya chai.
Bodi ya Chai Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi husika za Serikali pamoja na wadau wa sekta ya chai ili kutafuta suluhu la kudumu kwa changamoto hizo. Hatua hizi zinalenga kuboresha mazingira ya uzalishaji, kulinda maslahi ya wakulima na wafanyakazi, na kuhakikisha sekta ya chai inaendelea kuwa na mchango chanya katika uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.