Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

BODI YA CHAI TANZANIA

TBT yazinadi fursa za kibiashara kwenye sekta ya chai kwa Kampuni ya Hong Ding xin Investment ya Nchini China.

Imewekwa: 06 Dec, 2024
TBT yazinadi fursa za kibiashara kwenye sekta ya chai kwa Kampuni ya Hong Ding xin Investment ya Nchini China.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania (TBT) Bi. Beatrice Banzi amezinadi fursa za kibiashara kwenye sekta ya chai kwa Kampuni ya Hong Ding xin Investment ya Nchini China. 

Bi. Beatrice amezinadi fursa hizo katika kikao kilichoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya  Mazao, Dkt. Hussein Mohamed Omar, kilicholenga kuimarisha uwezezaji katika sekta ya chai hapa nchini.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ya China, Lai Huijun pia alikuwepo Mheshimiwa Mbunge Juma Nkamia, Hassan Ngaiza na Mtaalamu kutoka Idara ya Maendeleo ya Mazao- Wizara ya Kilimo,Bw. Yusuph Rajab.

Bi Beatrice amebainisha kuwa katika sekta ndogo ya chai hapa nchini zipo fursa nyingi za uwekezaji kama vile Viwanda vya Kuchata Chai, Viwanda vya Kuchanganya na Kufungasha Chai, pia  uwepo wa Mnada wa Chai Dar es Salaam nayo ni kati ya fursa  zilizopo.

Baada ya kutoa wasilisho lake hilo, wawekezaji hao wakiongozwa na Bw. Lai Luijun walibainisha kuwa wametembelea Mikoa na  Maeneo mbalimbali yanayolima chai na kusisitizia kuwa wamevutiwa kuwekeza katika Tasnia ya Chai hapa nchini.

Akizungumzia utayari wa Wizara ya Kilimo katika kushirikiana na Kampuni hiyo kuendeleza sekta ya chai, Naibu Katibu Mkuu amewahakikishia ushirikiano mzuri huku akiwakaribisha tena ofisini kwake pindi wakiwa tayari kuanza uwekezaji huo.