TBT YAFANYA MAZUNGUMZO NA UNDP KUHUSU KUENDELEZA SEKTA YA CHAI NCHINI
Timu ya Bodi ya Chai Tanzania (TBT) ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Bi. Beatrice Banzi, imefanya kikao na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara, pia ni muwakilishi wa Taasisi za kimataifa za UNCDF na UNV kilichofanyika katika Ofisi za UN jijini Dar es Salaam.
Lengo la kikao hicho ni kujadili njia za kuanzisha ushirikiano kati ya TBT na UNDP, UNCDF pamoja na UNV katika kukuza tasnia ya chai nchini Tanzania, hususan katika maeneo ya kuongeza ubunifu, thamani ya bidhaa (value addition) ili chai ya Tanzania ijulikane kimataifa.
Baadhi ya mambo muhimu yaliyo ongelewa kwenye kikao hicho ni kama ifuatavyo;
1. Fursa ya Ongezeko la watu nchini Tanzania ambapo inakadiriwa ndani ya miaka 15 idadi ya watu nchini inaweza kufikia watu milioni 100, hii inaweza kuwa chachu ya kufanya wawekezaji kufikiria kuinua sekta ya chai kwa kuzingatia matumizi ya zao hilo kwa soko la ndani na kuweza kupata faida kubwa.
2. Utalii kwenye Chai (Eco tourism) ambapo TBT na UNDP ilizungumza kwa upana ili kukuza sekta hii muhimu kwa kuitangaza kitaifa na kimataifa kupitia Eco tourism.
3. Kuanzisha mifumo ya kugharamia uwekezaji kwenye Chai mfano kuwa na Hati fungani (Bonds) za kuweza kugharamia miradi ya uwekezaji kwenye Chai. Hatua hii itapelekea watanzania kuweza kuwekeza miradi hii kwa fedha za ndani huku wakiwa wanategemea marejesho (Return on Investment) yanayotokana na uwekezaji huo, huku sekta ikiwa inajizalisha kibiashara.
4. Kuwekeza nguvu kwenye uongezaji thamani. Hatua hii itasaidia kuwa na aina mbalimbali za Chai zitakazokuwa zinashindana kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi yakiwa na vifungashio bora na vyenye kuvutia na ladha iliyotukuka
5. Kuwekeza nguvu kwenye Ubunifu (Innovations). Bw. Komatsubara ameieleza Bodi ya Chai kuwa wanafanya kazi kwa ukaribu na vijana wabunifu, hivyo wapo tayari kuwaunganisha na Bodi kwa ajili ya kuja na mipango mbalimbali ya ubunifu kwa ajili ya kuinua sekta hii muhimu.
6. Kutoa tuzo za ubora wa chai kwa wazalishaji. Katika hatua nyingine ya kuhimiza ubora wa Chai, Bodi na UNDP wataweka mpango wa kuanziaha mashindano ya kufahamu ubora wa chai kwa kulinganisha chapa mbalimbali za Tanzania. Hatua hii itapelekea kukuza chapa za Tanzania kwa wanunuzi pamoja na kukuza masoko ya Chai hizo kitaifa na kimataifa.
Pamoja na mambo mengine Bw. Komatsubara alieleza kuwa UNDP walishirikiana kwa ukaribu na wakulima wa nchi ya Malawi kwenye kuinua sekta yao ya Chai kwa kuanzia mfuko wa kilimo wa “Malawi Innovation Challenge Fund” ambapo anatamani kufanya hivyo kwa Tanzania pia ili kuweza kuinua sekta ya Chai.
Kwa Pamoja Bodi ya Chai na UNDP wamekubaliana kuandaa mpango wa pamoja utakaopitia hatua mbalimbali za kitaalamu utakaolenga kuinua sekta ya Chai. Vikao vya kujadili mpango huo vitaanza mara moja wiki hii ili kuweza kuja na jambo lenye tija kwa taifa. Ni matarajio ya Bodi kuwa mpango huu sio tu utainua sekta ya Chai bali utagusa maeneo mengi kama vile Ajira kwa wanawake, vijana, ukuaji wa sekta ya viwanda na mnyororo mzima wa thamani wa zao la chai.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai, Bi. Beatrice Banzi, alimshukuru Bw. Komatsubara kwa muda na nia njema aliyoonyesha katika kuendeleza sekta ya chai.
“Tunathamini sana ushirikiano huu na tutaendeleza mazungumzo haya kwa lengo la kuhakikisha sekta ya chai inazidi kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa Taifa,” alisema Bi. Banzi.
Kikao hicho kimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Bodi ya Chai Tanzania na UNDP katika kuinua sekta ya chai, kuongeza thamani ya bidhaa, na kuboresha masoko ya ndani na nje ya nchi.