Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

BODI YA CHAI TANZANIA

BODI YA CHAI YAKUTANA NA KAGLA VAPORTECH YA JAPAN KUJADILI TEKNOLOJIA YA VAPORIZER KWA VIWANDA VYA CHAI

Imewekwa: 07 Oct, 2025
BODI YA CHAI YAKUTANA NA KAGLA VAPORTECH YA JAPAN KUJADILI TEKNOLOJIA YA VAPORIZER KWA VIWANDA VYA CHAI

 Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania, Bi. Beatrice Banzi, amekutana na kufanya kikao na Naibu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Kagla Vaportech kutoka Japan, Bw. Hiro Shimanda, kampuni inayojulikana kwa utengenezaji wa vaporizers—mashine zinazobadilisha gesi ya LPG kuwa mvuke kwa matumizi ya viwandani.

Kikao hicho, kilichoongozwa na Bi. Banzi, kimehudhuriwa na wawakilishi kutoka Mponde Holding Company Limited, East Usambara Tea, Victoria Tea, EUTCO, Transform Trade, Vision Tea Brokers, Jamie Briquettes pamoja na maafisa wa Bodi ya Chai.

Lengo kuu la kikao hicho ni uhimizaji matumizi Ya nishati safi kwenye viwanda vya chai ambapo kampuni ya Kagla Vaportech imetoa elimu juu ya manufaa ya matumizi ya vaporizers katika viwanda vya chai, ikiwemo Kuimarisha udhibiti wa joto na kuboresha ubora wa chai, Kupunguza gharama za mafuta na matumizi ya kuni,Kuimarisha usalama wa mazingira na kupunguza uchafuzi wa hewa,Kuongeza ufanisi wa uzalishaji ili kuhakikisha chai bora inazalishwa kwa gharama nafuu na kwa wingi.

Wadau wengi wa sekta ya chai wameonesha kuvutiwa na teknolojia hiyo kutoka Japan na wameipongeza Bodi ya Chai kwa kuleta ugeni huo muhimu. Wamesema hatua hiyo itasaidia viwanda vya chai nchini kutumia nishati safi na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, jambo litakaloongeza ufanisi na ushindani wa chai ya Tanzania kwenye masoko ya kimataifa.