BODI YA CHAI TANZANIA YASHIRIKI KIKAO KATIKA OFISI YA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI INDIA

Bodi ya Chai Tanzania (TBT) imeshiriki kikao muhimu kilichofanyika katika ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini India, kilicholenga kujadili fursa za kibiashara na upanuzi wa masoko ya mazao ya kilimo kutoka Tanzania.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Balozi wa Tanzania nchini India, Anisa Kapufi Mbega, alisisitiza dhamira ya ubalozi kuendelea kushirikiana na taasisi za serikali ili kuhakikisha mazao ya Tanzania, hususan parachichi, chai na jamii za mikunde ikiwemo mbaazi, yanapata masoko mapya na yenye uhakika. Alibainisha kuwa India ni miongoni mwa wanunuzi wakubwa duniani wa bidhaa hizo na hivyo ni soko lenye nafasi kubwa ya kukuza ushirikiano wa kibiashara.
Kikao hicho kilihusisha taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko na Masoko ya Kilimo (COPRA), Taasisi ya Udhibitisho wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viwatilifu Tanzania (TPHPA), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
Vilevile, makampuni binafsi yaliyojitokeza ni pamoja na ETG, Kikombo Avocado Farm na SM Holding, yakionesha utayari wa kushirikiana katika kukuza usafirishaji wa bidhaa za kilimo kutoka Tanzania kwenda India.
Bodi ya Chai Tanzania iliwasilisha taarifa kuhusu hatua inazochukua kuhakikisha ubora na kuongeza thamani ya chai inayozalishwa nchini ili kuhimili ushindani wa soko la kimataifa. Aidha, TBT ilieleza mikakati ya kusaka masoko mapya ikiwemo kutumia maonesho ya kimataifa na mikutano ya kibiashara kama majukwaa ya kutangaza chai ya Tanzania.
Kwa upande wake, Balozi Mbega alieleza utayari wa ubalozi kushirikiana na taasisi za serikali na sekta binafsi ili kufanikisha malengo hayo, pamoja na kufungua mazungumzo na wadau muhimu wa biashara nchini India.
Kikao hiki kimeelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha diplomasia ya kiuchumi kati ya Tanzania na India, na kinatarajiwa kufungua milango ya fursa zaidi za kibiashara zitakazowanufaisha wakulima na wazalishaji wa mazao ya kilimo nchini.