Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

BODI YA CHAI TANZANIA

BODI YA CHAI YAFANYA MAZUNGUMZO NA UBALOZI WA MISRI KUIMARISHA SOKO LA CHAI YA TANZANIA

Imewekwa: 21 Nov, 2025
BODI YA CHAI YAFANYA MAZUNGUMZO NA UBALOZI WA MISRI KUIMARISHA SOKO LA CHAI YA TANZANIA

Bodi ya Chai Tanzania, ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Bi. Beatrice Banzi, imefanya kikao maalum katika  Ubalozi wa Misri jijini Dar es Salaam na kukutana na Balozi wa Misri nchini, Mhe. Sherif A. Ismail.

Mazungumzo hayo yamelenga kujadiliana juu ya fursa za kupanua soko la chai ya Tanzania nchini Misri ambapo ubalozi umepongeza ziara hiyo na kueleza kufurahishwa na ujio wa ugeni kutoka Bodi ya Chai, huku ukibainisha kuwa Misri ni miongoni mwa nchi zinazopenda kutumia chai kwa wingi kwani wastani wa unywaji chai (Per Capita tea consumption)
ni Kilomoja kwa kila mwananchi kwa mwaka.

Ofisi ya ubalozi imekubali kuwakaribisha Bodi ya chai kwenye makongamano mbali mbali ya biashara na uwekezaji kati ya nchi hiyo na Tanzania ambayo yatasaidia kufungua milango ya ushirikiano wa moja kwa moja katika biashara ya chai.

Vile vile Mhe.Balozi amemjulisha Mkurugenzi Mkuu kuwa ubalozi unatamani kuanzisha mashirikiano ya kibiashara kwenye maeneo mengi na kuweza kuingia makubaliano ya kurahisisha biashara hizo kwani Misri ipo chini ya Jumuiya mwanachama wa COMESA na Tanzania haipo, hivyo ni vizuri kuwa na makubaliano yatakayorahisisha ufanyikaji wa biashara kati ya nchi hizo mbili.

Aidha Bodi imewasilisha taarifa mbalimbali za sekta ya chai ikiwemo uzalishaji,uwekezaji na ubora wa chai ya Tanzania ili kuwezesha uchambuzi wa kina wa kibiashara kwa upande wa Ubalozi.

Biashara kati ya Tanzania na Misri ina historia njema, na kuimarisha biashara ya chai kutachangia kuongeza pato la mataifa yote mawili, kwani chai ya Tanzania imewavutia kutokana na ubora wake.