Warusi kuwekeza kwenye sekta ya chai nchini

Sera ya Diplomasia ya Uchumi inayohasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh,Dk. Samia Suluhu Hassan inazidi kuzaa matunda nchini.
Tangu kuingia madarakani miaka minne iliyopita, Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuinadi Tanzania kimataifa ikiwa ni pamoja na kutembelea na kushiriki mikutano mbalimbali mikubwa ya kimataifa kwa lengo la kuziangaza fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini.
Hatua hiyo imekuwa ikiwaleta nchini wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali ya ndani na nje ya Afrika.
Kati ya nchi hizo ni pamoja na Urusi ambapo mbali na kuwekeza hapa nchini kwa muda mrefu jana kupitia Balozi wake hapa nchini, jana imetangaza rasmi nia yake ya kutanua wigo zaidi wa uwekezaji kwa kuwekeza mkoani Iringa ikianza na sekta ya chai.
Ujumbe wa Urusi ukiongozwa na Balozi wake hapa nchini Mhe. Balozi Andrey Avetisyan pamoja na Mwakilishi kutoka Bodi ya Chai Tanzania(TBT), Bw. Lucian Kimaro upo mkoani Iringa kwa tatu kutembelea mashamba ya chai ya Mafinga na Njombe.
Akizungumzia uamuzi wa kuwekeza katika sekta ya chai nchini, Mhe. Balozi Avetisyan anasema kuwa Urusi imevutiwa na Sera ya Diplomasia ya Uchumi ya Rais Samia ambayo pamoja na mambo mengine imetangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya chai.
"Urusi na Tanzaniia tumekuwa na urafiki wa kidiplomasia na siasa kwa muda mrefu ila kwa sasa tunataka kujikita zaidi katika urafiki wa kiuchumi na hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania inajitangaza sana kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali" anasema Balozi huyo.
Amesisitiza kuwa Urusi inataka kuwekeza hapa nchini kwa mfumo shirikishi na wezeshi kwa kuwa ni njia nzuri ya kuendesha uchumi wa Tanzania badala ya kuwa watu wa kutoa misaada kama matrekta na bidhaa ambazo sio endelevu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa,Mh. Peter Serukamba amemhakikishia Balozi ushirikiano mzuri utakaotimiza adhma yao hiyo ya kuwekeza kwenye sekta ya chai mkoani Iringa.