KATIBU MKUU WA WIZARA YA KILIMO AAGIZA WAFANYAKAZI 216 WA WATCO KUREJESHWA KAZINI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli ameagiza kurejeshwa kazini wafanyakazi 216 wa Kampuni ya Wakulima Tea Company (WATCO) inayomiliki viwanda vya Katumba na Mwakaleli wilayani Rungwe, mkoani Mbeya.
“Tumekubaliana kuwa hakukuwa na sababu za msingi za kusitishwa kwa ajira za wafanyakazi hao, hivyo ni lazima wapewe barua zinazositisha kuondolewa kazini na Serikali inawahakikishia wafanyakazi hao kuwa ipo pamoja nao na inaendelea kushughulikia haki zao. Kwa sasa waendeelee na kazi kwa amani na utulivu na hakuna mfanyakazi atakayepoteza haki zake,” amesema Katibu Mkuu Mweli.
Amesema hayo tarehe 21 Oktoba 2025 jijini Dodoma wakati wa Mkutano wake na wamiliki wa kampuni ya WATCO; akiwemo mwakilishi wa wafanyakazi pamoja na chama cha wafanyakazi mashambani; na pia amesikiliza hoja kutoka upande wa Benki ya CRDB.
Aidha, Mkutano huo pia umewashirikisha Bw. Abdulmajid Nsekela, Mwenyekiti wa Bodi ya Chai Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB; na Bi. Beatrice Banzi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai ya Tanzania.
Mkutano huo ni mwendelezo wa kikao cha tarehe 13 Oktoba 2025 ambapo Katibu Mkuu Mweli alikutana na wadau hao kufuatia kuandamana kwa wafanyakazi wakidai kulipwa fidia kutokana na kusitishiwa ajira zao bila kupata stahiki wanazostahili kisheria.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Mweli amewahakikishia wakulima waliouza majani mabichi ya chai kwenye viwanda hivyo na ambao bado hawajalipwa; kuwa ndani ya wiki mbili mchakato wa malipo yao utaanza. Pia ameelekeza uongozi wa WATCO kuja na mpango wa kuwalipa wakulima hao mapema iwezekanavyo; na kukifufua kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na kuja na mpango unaoonesha kama WATCO inahitaji za uwekezaji ili wakopeshwe na benki ya CRDB ambayo ndiyo iliwakopesha fedha zao awali katika uwekezaji.
WATCO inatokana na umiliki wa asilimia 70 za wawekezaji; ambapo asilimia 30 zikimilikiwa na wakulima wenyewe.