Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

BODI YA CHAI TANZANIA

ITALIA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KUIMARISHA TASNIA YA CHAI.

Imewekwa: 15 Oct, 2025
ITALIA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KUIMARISHA TASNIA YA CHAI.

Katika jitihada za kuendeleza na kukuza tasnia ya chai nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania, Bi. Beatrice Banzi, amefanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mh. Giuseppe Seàn Coppola, kuhusu njia za kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kuvutia masoko ya kimataifa kwa zao la chai la Tanzania.

Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi za Ubalozi wa Italia zilizopo Upanga, Jijini Dar es Salaam, na yalihudhuriwa pia na PMO wa Bodi ya Chai pamoja na Mwambata wa Uchumi kutoka Ubalozi wa Italia.

Mheshimiwa Balozi Coppola ameelezea kufurahishwa kwake kukutana na uongozi wa Bodi ya Chai Tanzania na kupata uelewa wa kina kuhusu mnyororo wa thamani wa tasnia ya chai nchini.

Ameendelea kueleza kuwa kutokana na mafanikio ya Italia katika kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani wa zao la kahawa na kusaidia wakulima wadogo wa Tanzania, ni muhimu pia kufikiria ushirikiano mpana na Bodi ya Chai katika maeneo ya bidhaa mbadala na maendeleo ya viwanda vya kisasa.

Aidha, Mh. Balozi amebainisha kuwa sekta ndogo ya bidhaa za urembo zinazotengenezwa kwa chai (Tea Cosmetic Products) ni fursa nyingine muhimu ya ubunifu na biashara ambayo Italia inaweza kushirikiana nayo kwa karibu na Bodi ya Chai Tanzania.

Balozi wa Italia ameahidi kuendeleza mazungumzo na Bodi ya Chai Tanzania ili kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia ya kiuchumi kati ya Italia na Tanzania, hususan katika mnyororo mzima wa thamani wa zao la chai.